Leo ni Jumanne tarehe 19 Jamadil Awwal 1436 Hijria sawa na Machi 10, 2015.
Siku kama ya leo miaka 525
iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya
Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa
zama hizo alifariki dunia mjini Cairo. Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka
849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Jalaluddin Suyuti
kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya
Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa. Msomi huyo wa Cairo
ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah",
"Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa".
Tarehe 10 Machi miaka 139
iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani Alexander Graham Bell alivumbua simu na
siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na
msaidizi wake Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko
makubwa katika vyombo vya mawasiliano.
Bell alifaidika na uzoefu na
majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo
hicho cha mawasiliano ya haraka.
Baada ya hapo chombo cha simu
kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi
iliyofanywa na Alexander Graham Bell.
Tarehe 10 Machi siku kama ya
leo miaka 119 iliyopita jeshi la Italia lilishindwa vibaya katika
jaribio lake la kutaka kuivamia na kuikalia kwa amabavu Uhabeshi au
Ethiopia ya sasa. Lengo kuu la shambulizi hilo la Italia lilikuwa ni
kuiungunisha Ethiopia na makoloni mengine mawili ya nchi hiyo yaani
Somalia na Eritrea. Katika vita hivyo jeshi la Italia lilipata kipigo na
hasara kubwa ya hali na mali licha ya kuwa na silaha za kisasa na
kulazimika kurudi nyuma.
Na siku kama ya leo miaka 70
iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani
zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo.
Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha
mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu
wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika
mashambulizi hayo.
0 comments:
Post a Comment