Rais Kikwete: Unyonge CCM basi

 Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), mjini Dodoma

 Dodoma. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa chama hicho kuacha unyonge na kusema uvumilivu una kikomo chake.
Aliyasema hayo jana wakati anafungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, kilicholenga kuweka msimamo wa chama kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ambayo inaanza kujadiliwa Jumanne wiki ijayo.
“Tuna uchaguzi mdogo, Iringa, Kalenga, tumeshapata mgombea na tumefanya hiyo kazi kwa niaba yenu kwa sababu hatukupata muda wa kuitisha Kikao cha Halmashauri Kuu, lakini mmetupatia mamlaka ya kufanya hivyo na Katiba imetupa fursa ya kufanya uteuzi kwa niaba yenu,”alisema.
CCM imemteua Godfrey Mgimwa ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Dk William Mgimwa, kupeperusha bendera katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye mwaka huu. Dk Mgimwa hadi anafariki dunia alikuwa Waziri wa Fedha.
Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga lililopo mkoani Iringa unatarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka huu, huku tayari vyama vya CCM na Chadema vikiwa vimetaja wagombea wake, Chadema kikiwa kimetangaza, Grace Tendega Mvanda.
Rais Kikwete alisema chama hicho kinashindana na vyama vingine katika uchaguzi huo mdogo.
“Tunashindana na wenzetu wagomvi, maana wao ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa,”alisema Kikwete bila kutaja chama chochote cha siasa kwa jina.
“Tulizungumza nalo hilo kwenye Kamati Kuu, tulikubaliana kuacha unyonge. Ndiyo, kwenye Kamati Kuu tumekubaliana, tumesema jamani watu wote waende wakaseme tumekubaliana kuacha unyonge,” alisema huku akicheka na kupigiwa makofi na wajumbe wa Nec.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, alitolea mfano wa tukio lilitokea Kahama mkoani Shinyanga, ambapo kijana mmoja alitolewa macho kwa bisibisi, na tukio la Igunga ambapo kijana mmoja alimwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
“Acheni unyonge na hata katika taarifa ya habari leo (jana) mtoe hivyo hivyo. Na mwache habari zote mseme hii tu (waandishi wa habari). Uvumilivu una ukomo wake,” alisema huku wajumbe wakiendelea kumpigia makofi.
“Nalisema kwa sababu yanayotokea yanasikitisha sana. Pale Igunga kijana yule wamemwagia tindikali, pale Kahama kijana ametolewa macho kwa bisibisi,”alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwataka wanachama wa CCM kujipanga vizuri katika uchaguzi huo, ili kuhakikisha wanapata ushindi mnono.
Share on Google Plus

About nellychazzy

I Run And Own Nellychazy.blogspot.com. Working With Web Editing, Blogs Template Fix And Editing (HTML). Monitoring click4hosting.net Deals with Web hosting. Also Base On Software And Hardware, Phones,Computer
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Blogger Tricks