Kuhusu Chenge kuivimbia tume

Baraza la Maadili la Watumishi wa Umma jana lilishindwa kumhoji Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, baada ya kuwasilisha pingamizi la amri ya Mahakama Kuu inayodaiwa kuzuia mamlaka zozote kujadili au kulifanyia kazi suala lolote linalohusu kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji kifisadi wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Zuio hilo lilizua mvutano mkali wa kisheria baina ya wanasheria wa baraza hilo na Chenge, ambaye alilitadharisha kutokubali kuingia kwenye siasa, badala yake waiache majukwaani na washughulikie masuala ya msingi kisheria.
Chenge alidai ana maelezo ya kutosha ya tuhuma zilizoorodheshwa na baraza hilo dhidi yake, lakini kabla ya kuanza kujieleza ni vyema akapata mwongozo.
Mvutano huo ulizuka muda mfupi baada ya Mwanasheria wa Baraza hilo, Hassan Mayunga, kusoma hati yenye malalamiko 10 dhidi ya Chenge, yakiwamo ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Umma tangu akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995.
Baada ya kusomewa malalamiko hayo, Chenge aliomba mwongozo wa baraza akidai kuna zuio la mahakama kwa mamlaka zozote za serikali kushughulikia suala hilo.
MVUTANO ULIKUWA HIVI
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo. Malalamiko dhidi yangu chimbuko lake ni maamuzi ya Bunge katika mkutano wa 16 na 17. Ninavyofahamu mimi suala hili lipo mbele ya Mahakama Kuu na uamuzi umeshatoka kuwa mamlaka yoyote hairuhusiwi kushughulikiwa kwa namna yoyote ile,” alisema Chenge.
Aliongeza: “Hii ni ‘public document’ (waraka wa umma) bila mwongozo huo, mimi kama mwanasheria inanisumbua sana.”
Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu, Hamis Msumi, aliomba kuona zuio hilo.
Jaji Msumi: Naomba hilo zuio nilione…nimelisoma kwa uchache, je mnalo hili?
Mwanasheria Mayunga: Nimelisoma na halituzuii kuendelea na malalamiko yetu dhidi ya Chenge.
Mayunga alipinga mwongozo huo na kudai zuio la mahakama halihusiani kwa namna yoyote na malalamiko yaliyo mbele ya baraza dhidi ya Chenge.
“Tuhuma zilizopo mbele ya baraza ni ukiukwaji wa sheria na kanuni za maadili ya viongozi wa umma na siyo suala la kinachoendelea na kilichoelezwa katika zuio hilo, hivi ni vitu viwili tofauti,” alifafanua.
Mayunga alidai kwa mujibu wa Ibara ya 132 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sekretarieti ya Maadili ya Watumishi wa Umma inatajwa ikiwa  na mamlaka kamili ya kuhoji na kwa msingi huo iko huru na haipaswi kuingiliwa.
Alifafanua kuwa Sheria ya Maadili kifungu cha 18 (2) (c) inaeleza majukumu ya sekretarieti ambayo ni kuchunguza madai yoyote ya uvunjaji wa sheria ya maadili.
Mayunga alidai kuwa kifungu cha 4 kinatoa mamlaka kwa sekretarieti kuanzisha uchunguzi na ukiukwaji wowote wa maadili kulingana na matakwa ya sheria.
Alisema kifungu namba 29 cha sheria hiyo pia kinaeleza hakuna chombo kinachoweza kupunguza au kuzuia kufanya kazi yake na kwamba kwa vifungu hivyo Baraza hilo liko sahihi kuendelea na shauri hilo. Baada ya ufafanuzi huo, Chenge alisema anachofahamu hoja aliyoiwasilisha mbele ya baraza ni zuio lililopo Mahakama Kuu na kwamba iwapo chombo hicho (Baraza) kipo juu ya Mahakama hilo ni jambo jingine.
Hata hivyo, alitakiwa kusoma kipengele kimojawapo cha zuio hilo na kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili na alifanya hivyo huku akisisitiza moja ya kipengele ni kuhusu miamala ya benki iliyofanyika.
“Nionavyo chombo hiki (Baraza) kiheshimu amri halali iliyotolewa na Mahakama…unapokuwa katika hali kama hii Mamlaka ya chombo hiki yasiwe makubwa kushinda Mahakama Kuu…ni ushauri tu unaweza kuendelea kunihoji na maelezo ninayo ya kutosha,” alisema.
Aliongeza: “Utawala wa sheria uheshimiwe, masuala ya siasa yabakie kwenye majukwaa mengine yasiingizwe kwenye chombo hiki.”
“Kilichotajwa kwenye malalamiko dhidi yangu ni miamala ya benki ambayo imetajwa katika zuio la Mahakama, tusijifiche katika kichaka cha kusema sheria ya maadili inafanya kazi, suala hili lilianzia bungeni,” alisisitiza.
Mwanasheria wa Baraza, Filoteus Manula, alidai suala la ukiukwaji wa maadili haliendani na mashauri kama ya jinai, madai na rushwa, na kwamba kinachozungumziwa kwenye malalamiko ni ukiukwaji wa maadili aliyoyafanya tangu akiwa na wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa serikali. Mwanasheria mwingine wa Baraza, Getrude Cyriucus, alidai kuwa sekretarieti hiyo imepewa mamlaka ya kuanzisha uchunguzi bila kusubiri na wapo huru kuanzisha kuchunguza kupitia taarifa mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari.
“Tukiacha viongozi wa umma wajichagulie watakavyo, kamwe hatuwezi kufanya kazi yetu inavyotakiwa,” alidai.
Baada ya mvutano huo wa dakika 30, Chenge alisema alichoomba ni mwongozo na kuwasilisha mbele ya baraza zuio la mahakama, hivyo waamue kama wataendelea au la na kwamba ana maelezo ya kutosha dhidi ya tuhuma zilitotolewa dhidi yake.
Chanzo: NIPASHE
Share on Google Plus

About nellychazzy

I Run And Own Nellychazy.blogspot.com. Working With Web Editing, Blogs Template Fix And Editing (HTML). Monitoring click4hosting.net Deals with Web hosting. Also Base On Software And Hardware, Phones,Computer
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Blogger Tricks