Leo ni Jumapili tarehe 17 Jamadul-Awwal mwaka 1436 Hijria, sawa na tarehe 8 Machi 2015 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, inayosadifiana na 8
Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa
dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa
mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa
kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela.
Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za
Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa
Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka
1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na
serikali ya Manila.
Siku kama ya leo miaka 1145 iliyopita, yaani mwaka 291
Hijiria, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad bin Yahya, mtaalamu maarufu wa
lugha na nahau. Abul-Abbas katika masomo yake alibobea katika ulingo wa
fasihi ya Kiarabu na baada ya miaka kadhaa ya kufanya utafiti wa kina,
akatokea kuwa mtaalamu mkubwa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari
zilizobakia kutoka kwa mtaalamu huyo, ni pamoja na kitabu maarufu
kiitwacho ‘I’raabul-Qur’an’.
Siku kama ya leo miaka 986 iliyopita, alizaliwa Muhammad
Ghazali msomi wa fiq'hi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu wa Iran.
Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kwa Abu Nasri Ismail na alikuwa mmoja wa
wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo akiwa na umri wa miaka 28.
Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati
huo Khawaja Nidham al-Mulk kumualika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa
ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na
masuala ya ualimu. Imam Muhammad Ghazali aliandika kitabu chake maarufu
cha "Ihyau Ulumud-Din," mwaka mmoja kabla ya kurejea Iran. Vitabu
vingine mashuhuri vya msoni huyo ni "Kemia ya Saada" na "Nasaha za
Wafalme."
Na siku kama ya leo miaka 178 iliyopita, alizaliwa Sayyid
Muhammad Ali Shah Abdul-Adhim, maarufu kwa jina la ‘Hidaayat Husseini’,
faqihi na alimu mkubwa wa Kiislamu. Hidayat Husseini alisafiri mjini
Najaf, Iraq ambapo kwa miaka kadhaa alipata kusoma kwa Sheikh Murtadha
Answari, aliyekuwa mmoja wa mafuqahaa wakubwa katika ulimwengu wa
Kiislamu. Hidayat Husseini, alibobea katika elimu ya Hadithi na wapokezi
wa hadithi, huku akiandika vitabu vingi mojawapo kikiwa ni
‘Wasilatur-Ridhwaan’. Msomi huyo alifariki dunia mnamo mwaka 1343
Hijiria huko mjini Najaf.
0 comments:
Post a Comment