Serikali: Vituo vya watoto “feki” kufungwa


Serikali imesema haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanaotumia watoto wa mitaani kujinufaisha.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kitengo cha haki za mtoto na marekebisho ya tabia, Stephen Gumbo kwenye mkutano mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la kulea watoto la Kisedet mjini hapa.
Gumbo alisema kuwa, kuna baadhi ya watu hutumia watoto wa mitaani kufungua vituo kwa ajili ya kuwalea, lakini lengo lao likiwa ni kujipatia utajiri kupitia vituo hivyo.
“Utakuta watoto wanaishi maisha magumu, lakini yeye anajenga majumba na kuendesha magari ya kifahari kwa kutumia misaada anayoipata,” alisema Gumbo.
“Watoto wanadhalilishwa humo vituoni, wanapigwa, wananyanyaswa na hawapati huduma wanazostahili.”
Alisema kwenye vituo vingi vilivyopo, watoto hulala sehemu ambazo siyo salama na kuonya kuwa kama vituo hivyo vitabainika ni lazima Serikali itavifunga.
“Utakuta kituo kina jumla ya watoto 68, lakini magodoro yaliyopo ni saba tu. Ni lazima kituo kama hicho tukifungie na watoto tutawapeleka vituo vingine,” alisema Gumbo.
Alisema kwa kipindi kirefu Serikali haijafunga vituo hivyo, lakini kutokana na vingi kutokuwa na sifa, sasa vitafungwa.
Akizungumzia watu waliojitolea kulea watoto yatima, Gumbo alisema, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa mazingira mazuri ya kuwalea watoto hao na kuahidi kuwa Serikali itaviwezesha vituo hivyo.
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la Kisedet, Jacob Mhepe alisema, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi katika kulea watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kutokana na jamii kutokuwa na mwamko wa kuwasaidia.
Hatua ya Serikali kutaka kufunga vituo hivyo inaweza kuwa imechochewa na taarifa za hivi karibuni ambazo Jeshi la Polisi Dodoma lilifunga vituo vitatu katika eneo la Nkuhungu baada ya kubaini ukiukwaji wa taratibu.
Polisi walibaini kuwapo kwa watoto na vijana 115 kutoka mikoa 13, waliokuwa wakilelewa kwenye mazingira hatarishi.
Kubainika kwa watoto hao ni tofauti na matukio ya mkoani Kilimanjaro ambako polisi pia iliwabaini zaidi ya watoto 200 waliokuwa wamefungiwa kwa miaka takriban mitatu wakipewa mafunzo ya siri na hivyo kuibua hisia za ugaidi.
Chanzo: Mwananchi
Share on Google Plus

About nellychazzy

I Run And Own Nellychazy.blogspot.com. Working With Web Editing, Blogs Template Fix And Editing (HTML). Monitoring click4hosting.net Deals with Web hosting. Also Base On Software And Hardware, Phones,Computer
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Blogger Tricks