Profesa Lipumba: CCM ina wagombea wawili wa urais

Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Madai hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku tatu baada ya kujiuzulu uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu mgombea urais.
Akizungumza wakati akitangaza kujiuzulu wiki iliyopita, Profesa Lipumba alisema dhamira yake ilikuwa inamsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.
Juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka Kigali alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye wiki mbili zilizopita alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi ndani ya CCM ni mfumo  alisema katika kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha Ukawa, bali walikuwa tayari wameparaganyika.
“Ukweli ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu… mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo makubaliano hayo.
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kiuchumi.
Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii anatarajia kurejea nchini.
Agosti 6, mwaka huu Profesa Lipumba alijivua uenyekiti wa CUF wakati mkakati wa vyama vya upinzani kushirikiana kushika dola ukiwa umeshika kasi.
Chanzo: Mwananchi
Share on Google Plus

About nellychazzy

I Run And Own Nellychazy.blogspot.com. Working With Web Editing, Blogs Template Fix And Editing (HTML). Monitoring click4hosting.net Deals with Web hosting. Also Base On Software And Hardware, Phones,Computer
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Blogger Tricks