
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imejiondoa katika kesi ya kikatiba iliyoifungua Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga utekelezaji wa maazimio nane yaliyopitishwa na Bunge baada ya kushindwa kupinga mapingamizi yaliyowasilishwa na upande wa serikali.
Mbali na IPTL kampuni nyingine zilizohusika kupinga maazimio hayo ni Pan Africa Power Solution Ltd (PAP) mmiliki wa IPTL, Habinder Sethi (pichani), na mmiliki wa kamapuni VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.
Mbele ya Jaji Stella Mugasha, wakili wa upande wa utetezi, Gabriel Munyele, akisaidiana na wakili Joseph Sungwa, aliiambia mahakama kuwa hakuna haja ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwani zuio la muda waliloomba lilikuwa limeshaanza kutekelezwa na Bunge.
Upande wa serikali ukiongozwa na naibu Mwanasheria Mkuu, Gabriel Malata, ulidai kuwa ulipwe gharama za kesi kutokana na usumbufu uliofanywa na IPTL kung’ang’ania kupinga maazimio ambayo yalikuwa yalishaanza kutekelezwa. Malata alidai kuwa IPTL inatakiwa kulipa gharama za uendeshaji wa kesi zikiwamo uchapishaji wa majalada na muda waliotumia kuja mahakamani.
Aidha aliiomba Mahakama itumie vifungu vya sheria vinavyoelezea na masuala ya gharama za kesi kuiamuru IPTL kulipa gharama hizo. Malata aliiomba mahakama itende haki ili kukomesha usumbufu unaofanywa na kampuni au watu wanaofungua kesi wakati wakijua hawawezi kushinda.
Jaji Mugasha aliitaka kampuni ya IPTL iwajibike kwa kulipa gharama za kesi kwa kushindwa kujiondoa mapema kupinga maazimio hayo, huku wakijua fika yalishaanza kutekelezwa. Wakili Malata alisisitiza kuwa upande wa serikali utafuatilia ili kuhakikisha IPTL inalipa gharama za kesi kwa wakati mwafaka.
Chanzo: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment