ZIMEBAKI siku 15 kuchezwa kwa pambano la ngumi la uzito wa Welter kati ya mabondia mahiri Mmarekani Floyd Mayweather na Mfilipino Manny Pacquiao katika viunga vya Las Vegas , Nevada.
Floyd Mayweather na Manny Pacquiao
|
Mambo yafuatayo yanatarajiwa kuchomoza katika pambano hilo la karne kutokana na umahiri wa wakali hawa katika masumbwi.
‘Southpaw’
‘Southpaw’ ni bondia anayetumia mkono wa kushoto kufanya mashambulizi kwa mpinzani. Katika kivumbi hicho itashuhudiwa Pacquiao, ambaye ni mahiri wa kipengele hicho akikitumia vilivyo. Hali inaweza kuwa tofauti kwani Mayweather anajulikana kwa uharaka kuliko bondia yeyote kwa sasa pia Floyd anajulikana kwa uvumilivu anapoona makonde yanarushwa kwake.
Mayweather katika mapambano yake amefanikiwa kuondoa ndonga hatari 5 kwa wakali wa ‘southpaw’ ikikumbukwa mwaka 2013 alipomzabua mkali wa ‘mashoto’ Roberto Guerrero.
KO
Hakuna ubishi, macho ya wengi yanamtazama Pacquiao. Katika mapigano 57 aliyoshinda, 38 ameshinda kwa ‘knockout’ (KO). Pacquiao amewekwa kwenye orodha ya watupa makonde wagumu katika welterweight. Hata hivyo, tangu 2009 Pacquiao hajashinda pambano kwa KO.
Kwa upande wake Mayweather ameweka rekodi ya KO 26, pia ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2007 Floyd ameshinda KO moja alipomkung’uta Victor Ortiz mwaka 2011.
Utajiri
Haina kikwazo kwa wakali hawa kuhusu utajiri wao. Ripoti zinaonyesha kuwa Mayweather atajipatia kiasi cha dola milioni 150 huku Pacquiao akijinyakulia kwenye dola milioni 100 sawa na asilimia 60/40.
Jarida la Forbes limeandika: Mayweather ni mwanamichezo anayeongoza kwa kulipwa pesa nyingi dola milioni 105 mwaka 2013 ambaye yupo karibu yake ni msakata kabumbu Cristiano Ronaldo dola milioni 80.
Mapato ya Pacquiao, mwaka 2013 yalikuwa dola milioni 41.8 yaliyomweka katika nafasi ya 11.
Kilichopo Vegas
Mayweather ambaye anapaita Las Vegas nyumbani anafanya mazoezi akiwa na matumaini kuwa uenyeji wake utambeba siku hiyo.
Mapambano 10 ya mkali huyo yamepiganwa MGM, ni moja tu la mwaka 2005 lililochezwa nje ya mji huo, alimpomtandika Sharmba Mitchell katika Rose Garden, jijini Portland, Oregon.
Naye Pacquiao sio mgeni na mji huo, kwani amepanda ulingoni mara 11 MGM Grand, Aprili 2014 alimkandika Timothy Bradley.
Pambano la kwanza katika ulingo huo ilikuwa mwaka 2001 aliposhinda kwa TKO dhidi ya Lehlohonolo Ledwaba.
Kwa sasa Pacquiao anafanya mazoezi katika Wild Card Boxing Club, Hollywood maili 270 kutoka Las Vegas.
Takwimu zao
Mayweather ameonekana yupo sawa huku takwimu zake dhidi ya Marcos Maidana zikionyesha kuwa alitupa makonde 177 na yaliyofika sawasawa ni 102. Katika pambano la kwanza dhidi ya Maidana alitupa 274 na yaliyofika ni 178.
Pacquiao katika mchuano wake dhidi ya Chris Algieri alirusha makonde ya nguvu 60 yaliyofika sawasawa ni 43.
Pacquiao alipochuana na Bradley, alirusha 344 yaliyofika ni 148.
Umri na kustaafu
Pacquiao ana umri wa miaka 36, na miezi 9 na siku 23 akizidiwa na Floyd, 38.
Hata hivyo inaonyesha Maidana alipopambana mara ya pili na Mayweather aliachwa miaka 6.
Canelo Alvarez alipotua ulingoni dhidi ya Floyd alikuwa na umri wa miaka 23.
Sasa basi Manny Money (Floyd), Manny Man (Pacquiao) wote hawataki kuonyesha baada ya mchuano huo mkali watastaafu kutinga ulingoni labda mwishoni mwa mwaka.
Rekodi zisizovunjwaUshindi wa Mayweather wa mapigano 47 ni mzuri na unaovutia katika historia ya ndondi.
Mayweather anaweza kuwa sawa na mkali wa ‘heavyweight’, Rocky Marciano aliyeshinda mapigano 49-0
Mbaya alikuwa Julio Caesar Chavez kutoka Mexico miaka ya 1980-1993 akishinda 87-0
Hivyo basi Mayweather akimkung’uta Pacquiao kwa rekodi hizo hakuna atakayeshtuka.
0 comments:
Post a Comment