Sifa zimeendelea kumiminika kwa gazeti la Nipashe linalochapishwa na Kampuni ya The Guardian kuhusiana na ripoti zake za kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kwa kutoegemea upande miongoni mwa vyama vilivyosimamisha wagombea wa nafasi ya urais.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), kuanzia Agosti, mwaka huu, gazeti la Nipashe limekuwa likiripoti kwa haki na bila upendeleo habari zinazowagusa wagombea wa nafasi ya urais wakiwamo Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na Cuf.
Kadhalika, kituo cha televisheni cha ITV kimetajwa kutenda haki pia katika kuripoti kampeni zinazoendelea za uchaguzi mkuu. Gazeti la Nipashe na televisheni ya ITV ni vyombo vilivyo chini ya IPP.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa vyombo vya habari katika kuripoti habari za uchaguzi na hali ya usalama kwa wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema kinyume cha ilivyotarajiwa, vyombo binafsi kama Nipashe na ITV ndivyo vinavyoonekana kufanya kazi kama vyombo vya umma kwa kuzingatia usawa katika habari zao.
“Kinyume cha vile ilivyotegemewa, vyombo binafsi ndivyo hivi sasa vinaonekana kama vyombo vya umma kwa kuzingatia usawa katika habari zao,” alisema.
“Mtandao unavipongeza vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu binafsi kwa kuzingatia usawa katika kuripoti kampeni zinazoendelea za uchaguzi…wamefanya hivi bila kujali kama ni chama tawala, vyama vikubwa na vidogo. Ni ngumu kukosa taarifa zenye kujenga kwa wagombea wote, hasa katika nafasi za mbele za vyombo hivi,” alisema.
Olengurumwa alitolea mfano gazeti la Nipashe kwa kuonyesha matoleo ya wiki moja mfululizo kuthibitisha namna linavyojitahidi kutenda haki kwa wagombea wote. Gazeti jingine lililoelezewa kuwa linaripoti habari za uchaguzi mkuu kwa haki ni Mwananchi.
Kadhalika, Olengurumwa alizungumzia pia namna ITV inavyotenda haki kwa kutoa nafasi kwa wagombea wote.
“Tumefuatilia kwa karibu taarifa za habari za ITV. Wanatoa nafasi kwa wagombea wote na wanapishana kwa zamu. Kama mmoja ataanza leo, kesho ni mwingine… tumeona hadi mgombea urais wa Chaumma, Hashimu Rungwe, anapewa muda mrefu licha ya kwamba mikutano yake haina mafuriko kama ya wagombea wa CCM na Ukawa,” alisema.
Alisema vyombo vya umma vinaripoti kampeni za uchaguzi kwa kupendelea chama tawala na kuvipa nafasi ndogo vyama vya upinzani, huku wakati mwingine kutovipa nafasi kabisa au kuripoti habari za kuvichafua peke yake.
“Kwa kufanya hivi, vyombo hivi vimejigeuza kuwa vyombo vya serikali na CCM badala ya kuwa sauti ya umma ambayo ndiyo walipa kodi…magazeti ya umma yanaonyesha waziwazi kuipendelea CCM kwa kuipa nafasi kubwa ya mbele, huku vyama vingine vikipewa nafasi ndogo ama kutopewa kabisa na wakati mwingine taarifa za upinzani kuonekana ni zile zenye mrengo hasi,” alisema.
Huku akionyesha magazeti yaliyoripoti vizuri na yenye kuegemea upande mmoja, Olengurumwa alisema matoleo mengi ya magazeti ya umma yanaonyesha taarifa nyingi hasi dhidi ya Ukawa, huku wagombea wa CCM wa nafasi ya urais na mgombea mwenza wake na pia watu wao wa kampeni wamekuwa wakipewa nafasi kubwa na taarifa za kuwajenga.
“Pia kumekuwa na taarifa zinazolenga kukandamiza chama au mgombea wa mrengo fulani kwa maslahi ya chama fulani, huku vipindi vingi maalum pamoja na vile vya moja kwa moja (live) vimekuwa vikionekana kupendelea CCM, hasa wagombea urais na timu yake,” aliongeza kusema.
Aidha, alitoa wito kwa vyombo vya habari na wanahabari nchini kuzingatia usawa na maadili ya taaluma zao katika kuripoti kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini. Mbali na Nipashe, ITV na vyombo vingine vya habari vya ITV, utafiti huo wa THRDC ulijumuisha pia Azam Tv, Mwananchi, Habari Leo, Daily News, Uhuru na Tanzania Daima.
Pongezi hizo kwa Nipashe zimetolewa ikiwa ni siku chache tu baada ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), kulitaja pia gazeti hili kuwa miongoni mwa yanayoripoti vyema habari za uchaguzi mkuu kwa kutoegemea upande wowote.
Chanzo: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment