Gwajima: Kikwete wakemee polisi


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye anawatuma.
Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo jana, Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.
“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa… asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.
Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.
Uraia wake
“Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa,” alisema.
Alisema makundi ya jamii yamekuwa yakitoa kauli mbalimbali lakini hayabughudhiwi anavyofanyiwa.
“Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana,” alisema.
Kuhusu utajiri wake
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya waumini. Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.
“Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata wapi?” alisema na kisha kuwauliza waumini hao… “Hivi baba yenu nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?”
Alijibiwa, “Tutakupaaaa!” Baada ya majibu hayo waumini hao walianza kupeleka fedha katika jukwaa kuu huku wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu.
Chanzo: Mwananchi
Share on Google Plus

About nellychazzy

I Run And Own Nellychazy.blogspot.com. Working With Web Editing, Blogs Template Fix And Editing (HTML). Monitoring click4hosting.net Deals with Web hosting. Also Base On Software And Hardware, Phones,Computer
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Blogger Tricks